Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetumia muda mrefu kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadau wengine ili kuwezesha Mchezo wa Marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la TotalEnergies CAF 2024/25 kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam tarehe 25 Mei 2025.
Jitihada hizi ni sehemu ya utekelezaji wa sera mpya iliyotangazwa miaka michache iliyopita na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, inayolenga kuielekeza Sekretarieti ya CAF kushirikiana na kusaidia kwa njia zote zinazowezekana, kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, utawala bora na haki, kuhakikisha kila Klabu ya Soka na Timu ya Taifa katika nchi 54 wanachama wa CAF inacheza katika uwanja wa nyumbani uliochaguliwa na kupendekezwa na uongozi wa shirikisho la soka la nchi husika na klabu.
Sera hii ni sehemu ya malengo ya Rais Motsepe ya kukuza, kuendeleza na kuimarisha soka la Klabu na Timu za Taifa katika kila nchi mwanachama wa CAF, pamoja na kuhakikisha zinaweza kujitegemea kifedha kwa muda mrefu.
CAF inatoa shukrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais wake Wallace Karia, pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania kwa mikutano na majadiliano yaliyofanyika, mchango wao na juhudi zao katika kusaidia Uwanja wa Benjamin Mkapa kutimiza matakwa na viwango vya CAF.
Hata hivyo, kutokana na changamoto ya muda, ripoti ya kampuni huru ya kimataifa inayotathmini viwanja ilibainisha kuwa ukarabati muhimu na maboresho yaliyohitajika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa hayawezi kukamilika kwa wakati kabla ya tarehe ya mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho la TotalEnergies CAF 2024/25, uliopangwa kuchezwa tarehe 25 Mei 2025. Kama ilivyotangazwa awali na CAF kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, mchezo huo sasa utafanyika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
CAF inasisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na TFF, Serikali ya Tanzania na wadau wote kuhakikisha kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na viwanja vingine pamoja na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya mashindano ya TotalEnergies African Nations Championship (CHAN) Kenya, Tanzania, Uganda 2024 vinakidhi viwango na masharti ya CAF. Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza tarehe 2 Agosti 2025, na CAF ina matumaini makubwa kuwa yatafanyika kwa mafanikio makubwa.